Swahili New Testament Bible

2nd Corinthians 3

2 Corinthians

Return to Index

Chapter 4

1

 Basi, Mungu, kwa huruma yake, ametukabidhi kazi hii na hivyo hatufi moyo. 


2

 Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali tunaudhihirisha ukweli kwa kuufanya ukweli, na hivyo kujiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele ya Mungu. 


3

 Maana, kama Habari Njema tunayohubiri imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea. 


4

 Hao hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni mfano kamili wa Mungu. 


5

 Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. 


6

 Mungu ambaye alisema, "Mwanga na uangaze kutoka gizani," ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo. 


7

 Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe. 


8

 Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; 


9

 twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa. 


10

 Kila wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu pia udhihirike katika miili yetu. 


11

 Naam, katika maisha yetu yote tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa. 


12

 Hii ina maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya kazi. 


13

 Maandiko Matakatifu yasema: "Niliamini, ndiyo maana nilinena." Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena. 


14

 Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi. 


15

 Yote haya ni kwa faida yenu; ili kama vile neema ya Mungu inavyoenea kwa watu wengi zaidi na zaidi vivyo hivyo watu wengi zaidi watoe shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu. 


16

 Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. 


17

 Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu: lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. 


18

 Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele. 


2nd Corinthians 5

 

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: